Friday, October 1, 2010

WAANDISHI WA HABARI WAWILI WASHAMBULIWA

*      Hii ni dalili mbaya kwa kazi za kuihabarisha jamii na taaluma kwa ujumla
*      Hofu yatanda kwa waandishi wengine kanda ya magharibi ambako zipo issues nyingi za maendeleo

Katika kile kinachodhaniwa kuwa ni kuzima harakati za wanahabari na vyombo vya habari kusaidia jamii kujua masuala mabali mbali ya maendeleo na hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi, waandishi wa habari wawili wanaofanya kazi katika jiji la Mwanza nchini Tanzania hivi karibuni wameshambuliwa huku mmoja akiswekwa ndani kwa agizo la kiongozi mmoaj wa serikali.

Dhahama hilo linaloenda kinyume cha katiba ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania ibara ya kumi na nane inayotoa uhuru wa kutoa au kupata habari, limemkumba mwakilishi wa idhaa ya kishwahili ya BBC London Bw. Erick David Nampesya, pamoja na Mwandishi wa magazeti ya Mwananchi Communication Bw. Fredrick Katulanda naye ameonja joto la jiwe mara tatu mfululizo, ambapo anataja kuwa alishambuliwa na watu wasio julikana nyumbani kwake na kasha kutoweka bila kupora chochote zaidi ya suluba dhidi ya mwili wake.

Akiongea na Kigoma Leo kwa njia ya simu, Erick David anaeleza kuwa alishambuliwa na mgambo wa jiji la mwanza na kisha kusweka rupango kwa agizo la mkurugenzi wa jiji la mwanza Bw. Wilson

Bw. Nampesya ameeleza kuwa kilichotokea ni mkurugenzi wa jiji kuchukizwa na habari iliyotangazwa na BBC kuhusu shule nyingi za msingi katika jiji la Mwanza kutokuwa na vyoo hali inayohatarisha afya za watoto na kushuka pia kwa kiwango cha elimu katika jiji hilo.

Na kana kwamba haitoshi mwandishi Fredrick Katulanda hivi karibuni yeye aliambulia kichapo pale alipokuwa wakifuatilia mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu hapa nchini.

Bw. Katulanda amedai kufuatiliwa na watu asio wajua na kwamba siku moja akiwa nyumbani alivamiwa na kupigwa na watu wapatao wanne na kisha kutoweka bila kujulikana.

Amebainisha kuwa katika tukio la pili alizuiliwa kuendelea na msafara wa kampeni za mgombea Urais wa chama cha mapinduzi DR. Jakaya Kikwete katika mikkoa ya kanda ya ziwa, ingawa ametaja kuwa kitendo hicho hakikutokana na amri ya Kikwete bali wapambe wake.

Katika tukio jingine, Bw. Katulanda alipigwa na kufukuzwa eneo la mkutano wa kampeni za chama cha mapinduzi mkoani Mwanza baada ya kiongozi mmoja wa chama hicho kuwaamuru vijana wa CCM maarufu kwa jina la Green Guard kuwafukuza waandishi wa habari katika mkutano wao na pale walipotaka kujua sababu za kufukuzwa, ndipo walipotandika na kulazimika kukimbilia polisi

Matukio haya ya kupigwa au kuzuiliwa kuandika habari kunakowatokea wanahabari Tanzania ni matokeo ya uwajibikaji mdogo wa viongozi ambao wanaposhindwa kutimiza wajibu wao kwa wananchi hutafuta mbinu za kuzuia maovu yao yasiangazwe.

Sunday, September 26, 2010

UHARAMIA ZIWA TANGANYIKA NA ATHARI ZA MAISHA NA UCHUMI KIGOMA

Na. Prosper Kwigize
Kigoma

Shughuli za uvuvi wa dagaa na samaki ndani ya ziwa Tanganyika zimezorota kwa kiwango kikubwa kutokana na vitendo vya kiharamia vinavyotajwa kuongezeka katika ziwa hilo mkoani Kigoma  na kutishia ustawi wa wavuvi na shughulii nyingine za kiuchumi na kijamii zinazofanywa ndani ya ziwa hilo linalounganisha nchi za Burundi, DRC na Zambia

Kwa mujibu wa wavuvi wanaoendesha shughuli zao ndani ya ziwa hilo, vitendo vya uvamizi, utekaji na uporaji vinavyofanywa na uharamia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku na kusababisha wavuvi kuporwa engine za boti na bidhaa nyingine ndani ya ziwa hilo, sambamba na kusababisha vifo na majeraha kwa wavuvi.

Hadi sasa inatajwa kuwa takribani ingine 24 za mitumbwi ya wavuvi kutoka kigoma zimeporwa na maharamia wenye ushirikiano kutoka Tanzania, DRC na Burundi na hivyo kutia hofu wavuvi na kuchangia bei ya dagaa na samakai wanaovuliwa ndani ya ziwa hilo kupanda kwa asilimia mia moja.

Ibrahimu Sendwe ni makamu mwenyekiti wa chama cha wavuvi mkoani Kigoma, yeye anabainisha kuwa vitendo vya uharamia ndani ya ziwa Tanganyika vinashamili kutokana na kutokuwepo kwa doria thabiti za vyombo vya ulinzi ziwani na hivyo kutoa mwanya kwa maharamia kuteka, kupora na kasha kutoweka bila kukamatwa na polisi.

Bw. Sendwe anaeleza kuwa, wavuvi ndani ya ziwa Tanganyika wamekuwa wakikabiriwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na ulinzi hafifu na kwamba licha ya jeshi la polisi kupata taarifa za uharamia unaofanyika ziwani humo, msaada unaotolewa ni hafifu.

“Maharamia wanaotusumbua wanatoka DRC, wamekuwa wakiteka na kupora mali zetu hasa injini za mitumbwi na kusafiri nazo hadi nchini kwa bila kukamatwa, na serikali zote mbili Tanzania na Congo zinajua uwepo wa tatizo hili, tunaashangaa hakuna hatua zinazochukuliwa na mabalozi wetu” Anasisitiza Bw. Sendwe, makamu mwenyekiti wa wavuvi mkoani Kigoma.

Bw. Sendwe amebainisha kuwa tayari chama chao kimepata taarifa kuwa injini 24 zilizoporwa na maharamia na kusafirishwa kwenda DRC zimekamatwa na kwamba wavuvi wa Kigoma wanaandaa utaratibu wa kimataifa kwenda kuzirejesha inijini hizo.

Mkuu wa jeshi la polisi mkoani Kigoma kamishina msaidizi wa polisi George Mayunga alipoulizwa kuhusu uharamia huo wa ziwani Tanganyika alisema kuwa, takribani matukio makubwa matano ya uharamia yametokea katika kipindi cha miezi sita na kwamba wapo maharamia wanaoshikiria kwa uchunguzi ili kulibaini kundi lao.

Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Kigoma Mrakibu mwandamizi wa Polisi Bw. Joseph Konyo anatoa taarifa kwa niaba ya mkuu wa polisi mkoa wa Kigoma, kwamba mwezi june mwaka huu matukio makubwa mawili ya uporaji wa ingine ulifanyika na Jeshi lilifanikiwa kumkamata haramia mmoja kutoka jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ambaye hadi sasa yuko rumande akisubiri kujibu mashataka kadhaa ya kuingia nchini na kufanya uharamia.

“Tunayo mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunaukomesha uharamia na hivi karibuni tumeanza kufanya mazungumzo ya kiintelijensia baina yetu na serikali ya Burundi, kwa kushirikisha vikosi vya ulinzi na usalama na tayari yapo makubaliano kadhaa ambayo yamefikiwa hasa kuhusiana na ubadirishanaji wa taarifa za kiusalama” Anasema Joseph Konyo mkuu wa upelelezi mkoa wa Kigoma.

Hivi karibuni Rais
wa Tanzania Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mkoani Kigoma kwa shughuli za kujinadi ili apatiwe fursa nyingine ya kuiongaza Jamhuri ya muungano wa Tanzania, na katika ahadi zake alieleza kuwepo kwa mikakati ya kupambana na maharamia ndani ya ziwa Tanganyika.

Rais Kikwete alieleza kuwa, tayari serikali za Tanzania na Marekani zimeingia katika ushirikiano kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa askari za kikosi cha doria katika ziwa Tanganyika, Victoria na Bahari ya hindi kwa lengo la kukomesha uharamia unaoendelea hadi sasa.

Alieleza kuwa tayari askari kadhaa wamesafirishwa kwenda marekani kwa ajili ya mafunzo na serikali inatengeneza Boti kadhaa kwa ajil ya shughuli za ulinzi na usalama katika maziwa hayo mawili ya kasikazini Magharibi mwa Tanzania.

Pamoja na shughuli nyingine za kilimo na ufugaji, wakazi wa mkoa wa kigoma hususani wilaya za Kigoma vijijini na Kigoma mjini wanalitegemea ziwa Tanganyika kwa shughuli za kiuchumi hususani uvuaji wa dagaa na samaki aina ya mgebuka, hivyo endapo ulinzi hautaimarishwa ni wazi kuwa uchumi wa wavuvi na wafanyabiashara wanaolitumia ziwa hilo kwa shughuli za usafiri na usafirishaji utaporomoka.


Wednesday, September 22, 2010

TAKUKURU YAPIGA MKWARA WAANDISHI WA HABARI KIGOMA, TABORA, SINGIDA NA DODOMA

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Tanzania imetoa tahadhari kwa waandishi wa habari watakaokiuka kanuni za maadili na sheria ya kuzuia Rushwa na sheria ya uchaguzi kuwa haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kama wakosaji wengine.

Tahadhari hiyo imetolewa na mkuu wa taasisi hiyo mkoa wa Dodoma Bi. Eunice Mmari wakati akifungua mkutano wa siku moja wa waandishi wa habari kutoka miko aya Kigoma, tabora, Singida na Dodoma iliyofanyika katika hoteli ya Dodoma Hotel jumanne wiki hii.

Bi. Mmari alieleza kuwa taifa linawatarajia sana wanahabari katika kuelimisha jamii kuhusu masuala mbalimbali ya kutimiza wajibu kwa jamii na viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wapiga kura wakati wa uchaguzi na hivyo isingekuwa vema wana habari nao kuhusika katika kukiuka sheria.

Alisisitiza kuwa baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakilaumiwa kwa kuomba fedha kutoka kwa wadau ili waandike habari zao jambo ambalo ni kinyume cha sheria ya gharama za uchaguzi namba sita na sheria ya Rushwa namba 11 ya taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania.

Bi. Mmari alisisitiza kuwa vyombo vya habari ni mmhimili mkubwa sana na tarajio la taifa katika kujenga maadili katika jamii na miongoni mwa watumishi wa umma, hivyo ni vema wakazingatia kanuni za maadil wakati wa kuandika na kuripoti habari za uchaguzi mkuu wa wabunge, madiwani na rais mwaka huu wa 2010.

Kwa upande wao wanahabari walioshiriki mafunzo hayo, wametaja changamoto m,balimbali zinazowakabiri mikoani katika kuandika habari za uchaguzi na kutaja kuwa vyombo vya habari na wamiliki wake havitoi kipaumbele kwao tofauti na wanavyofanya kwa waandishi walioko Dar es salaam.

Wanahabari hao wamelalamikia pia vitendo vya baadhi ya wahariri kuegemea vyama au wagombea na kupelekea habari zinazoandikwa kutoka mikoani dhidi ya wagombea au vyama Fulani kutoandika magazetini au kutangazwa katika radio na Runinga.

Aidha wameonya kuwepo kwa wamiliki wa habari ambao ni wadau wa kisiasa na wadhamini wa vyama ambao huwataka wahariri wao kutoandika habari za mgombea au chama fulanai na kushirikiza vyombo vyao kuvitangaza vyama vingine zaidi kuliko vyama vya wapinzani wao.

Mafunzo ya kanuni za maadili ya uandishi wa habari za uchaguzi mwaka huu yalidhaminishwa na mpango wa elimuya uchaguzi chini ya shirika la mapango wa maendeleo duniani UNDP na kuhudhuriwa na wanahabari zaidi ya arobaini kutoka kanda ya kati na magharibi.

Mwisho.

Saturday, September 18, 2010

MABOMU YA KIVITA YAKUTWA KATIKA MAKAZI YA WATU KIGOMA


Mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono yameokotwa jana katika mtaa wa Mwenge kata ya Gungu mjini Kigoma yakiwa yamehifadhiwa juu ya mti wa Mrumba ulio katikati ya nyumba tatu katika eneo hilo .

Mashuhuda wa tukio hilo ,wamesema mabomu hayo yaligunduliwa na vijana wawili waliopewa kazi ya kukata mti huo, ambapo wakiwa wanaendelea na kazi hiyo waligundua kuwepo kwa mfuko uliopachikwa katika moja ya matawi.

Shuhuda huyo Bakili Mohamed  amesema baada ya kuona mfuko huo,waliushika na kuushusha chini lakini hawakuvitambua vitu vilivyokuwemo hadi watu walipokusanyika zaidi na kugundua kuwa ni mabomu,hali iliyofanya waite polisi.

“Leo ilikuwa mwisho wa uhai wetu,tumeyashikashika kwa mikono kidogo,na hatukujua kama ni mabomu hadi alipokuja mama mmoja na kusema hiyo ni hatari hayo ni mabomu nyie vijana iteni polisi haraka tutakufa wote”alisema Bakili.

Baada ya kupata taarifa hiyo,jeshi la polisi lilitoa taarifa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ ambao walifika katika eneo hilo na kuyachukua mabomu hayo ambayo yalikuwa bado hayajalipuka.

Mti yalipokutwa mabomu hayo upo katikati ya nyumba ya Hamidu Mohamed,Isabela January na Kani Okange,ambapo vijana hao walipewa kazi ya kukata mti huo na mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo Hamidu Mohamed.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma George Mayunga amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba limewahoji vijana wawili Bakila Mohamed na Yahya Ramadhan ambao walipewa kazi ya kukata mti huo na kuwaachia.

“Tunawashukuru sana wananchi,wameona vitu wasivyovifamu na wametuarifu haraka na sisi tumechukua hatua zinazostahili bila kuchelewa kwa kushirikiana na wenzetu wa Jeshi la Wananchi”alisema kamanda Mayunga.

Hata hivyo amesema polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha mabomu hayo kuhifadhiwa katika mti huo.


Na. Propser Kwigize, Kigoma leo

AJALI ZA BARABARANI ZINAVYOUA NGUVU KAZI MKOANI KIGOMA

Jumla ya watu hamsini na sita wakiwemo abiria na madreva wa magari wamepoteza maisha katika ajali za barabarani katika kipindi cha January 2009 hadi june 2010 katika mkoa wa Kigoma nchini Tanzania na kupelekea taifa kupoteza nguvu kazi na kushuka kwa uchumi wa kaya za marehemu.

Kwa mujibu wa kitengo cha usalama barabarani cha jeshi la polisi Tanzania ajali zilizosababisha vifo vya watu hao zilitokana na ubovu wa miundombinu ya usafiri ikiwemo barabara pamoja na uzembe au uchakavu wa magari yanayotumiwa na ab iria kwa ajili ya safari.

Mkuu wa usalama barabarani mkoa wa Kigoma ASP William Mkonda ameeleza kuwa katika kipindi cha mwaka 2009 jumla ya ajali zilizotokea zilikuwa 379 wakati akatika kipindi cha January hadi june 2010 tayari ajali 380 zimetokea

Bw. Mkonda ameeleza kuwa abiria waliopoteza maisha ni 42 wakati amdeva walifariki tisa hadi june mwaka huu na kwamba uaharibifu mkubwa wa mali umetokea ikiwa ni pamoja na kusababisha majeruhi kufikia idadi ya watu 90.

Mkuu huyo wa usalama barabarani mkoa wa Kigoma amefafanua kuwa licha ya uzembe wa abiria, madereva na wamiliki wa magari, ajali nyingine hutokana na waenda kwa miguu na watumiaji wengine wa vyombo vya moto hususani pikipiki pamoja na baiskeli.

Jumla ya waendesha pikipiki 7 na waendesha baiskeli 6 wameripotiwa kufariki dunia katika matukio mbalimbali ya ajali za barabarani mkoani Kigoma, wakati waliojeruhiwa wakitajwa kuongezeka siku hadi siku kutokana na ajali za pikipiki.

Aidha ukosefu wa elimu ya usalama barabarani ni moja ya changamoto zinazoukabiri mkoa wa kigoma katika suala la matumizi ya barabara na vyombo vya usafiri.

Kutokana na changamoto hizo jeshi la polisi limeelezea azima yake ya kuanzisha mkakati wa ukaguzi madhubuti wa magari kabla ya safari pamoja na utoaji wa elimu kwa abiria na madereva, na kwa wanafunzi katika shule za msingi na sekondari ili kupunguza ajali za barabarani.

Tuesday, September 7, 2010

HOFU YA POLIO MKOANI KIGOMA

Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na shirika la afya duniani, limebaini kuwepo kwa uwezekano wa kuibuka kwa maambukizi ya ugonjwa wa polio katika mipaka ya Tanzania na jamhuri ya Kidemohrasia ya Kongo DRC.



Akiongea na Channel afrika kwa njia ya simu, Mganga mkuu wa Mkoa wa Kigoma Dr. Valentino Bangi amebainisha kuwa kutokana na mawasialiano ya ujirani mwema pamoja na ukaguzi wa taarifa mbalimbali za kiafya katika mipaka hiyo, serikali ya Tanzania imepata taarifa kuwa nchini DRC kuna maambukizi ya Polio.



Dr. Bangii amebainisha kuwa kutokana na taarifa hizo, wizara ya afya kwa kushirikiana na WHO wameandaa mkakati kabambe wa kutoa chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano katika wilaya ya Kigoma inayopakana na DRC mwambao wa ziwa Tanganyika.



Amesema kiasi cha dozi laki moja cha chanjo ya polio kimekwisha wasili mkoani Kigoma na zoezi la uchanjaji lilianza jumamosi August 21, 2010.



Kwa upande wake idara ya afya katika bandari ya Kigoma inayotoa huduma za usafiri na usafirisdhaji wa mizigo kwenda DRC, Burundi na Zambia, imeelezwa kuwa maafisa wa afya wamejiweka tayari kukagua na kutoa chanjo kwa abiria watoto wanaoingia nchini Tanzania.