Sunday, September 26, 2010

UHARAMIA ZIWA TANGANYIKA NA ATHARI ZA MAISHA NA UCHUMI KIGOMA

Na. Prosper Kwigize
Kigoma

Shughuli za uvuvi wa dagaa na samaki ndani ya ziwa Tanganyika zimezorota kwa kiwango kikubwa kutokana na vitendo vya kiharamia vinavyotajwa kuongezeka katika ziwa hilo mkoani Kigoma  na kutishia ustawi wa wavuvi na shughulii nyingine za kiuchumi na kijamii zinazofanywa ndani ya ziwa hilo linalounganisha nchi za Burundi, DRC na Zambia

Kwa mujibu wa wavuvi wanaoendesha shughuli zao ndani ya ziwa hilo, vitendo vya uvamizi, utekaji na uporaji vinavyofanywa na uharamia vimekuwa vikiongezeka siku hadi siku na kusababisha wavuvi kuporwa engine za boti na bidhaa nyingine ndani ya ziwa hilo, sambamba na kusababisha vifo na majeraha kwa wavuvi.

Hadi sasa inatajwa kuwa takribani ingine 24 za mitumbwi ya wavuvi kutoka kigoma zimeporwa na maharamia wenye ushirikiano kutoka Tanzania, DRC na Burundi na hivyo kutia hofu wavuvi na kuchangia bei ya dagaa na samakai wanaovuliwa ndani ya ziwa hilo kupanda kwa asilimia mia moja.

Ibrahimu Sendwe ni makamu mwenyekiti wa chama cha wavuvi mkoani Kigoma, yeye anabainisha kuwa vitendo vya uharamia ndani ya ziwa Tanganyika vinashamili kutokana na kutokuwepo kwa doria thabiti za vyombo vya ulinzi ziwani na hivyo kutoa mwanya kwa maharamia kuteka, kupora na kasha kutoweka bila kukamatwa na polisi.

Bw. Sendwe anaeleza kuwa, wavuvi ndani ya ziwa Tanganyika wamekuwa wakikabiriwa na changamoto mbalimbali zinazotokana na ulinzi hafifu na kwamba licha ya jeshi la polisi kupata taarifa za uharamia unaofanyika ziwani humo, msaada unaotolewa ni hafifu.

“Maharamia wanaotusumbua wanatoka DRC, wamekuwa wakiteka na kupora mali zetu hasa injini za mitumbwi na kusafiri nazo hadi nchini kwa bila kukamatwa, na serikali zote mbili Tanzania na Congo zinajua uwepo wa tatizo hili, tunaashangaa hakuna hatua zinazochukuliwa na mabalozi wetu” Anasisitiza Bw. Sendwe, makamu mwenyekiti wa wavuvi mkoani Kigoma.

Bw. Sendwe amebainisha kuwa tayari chama chao kimepata taarifa kuwa injini 24 zilizoporwa na maharamia na kusafirishwa kwenda DRC zimekamatwa na kwamba wavuvi wa Kigoma wanaandaa utaratibu wa kimataifa kwenda kuzirejesha inijini hizo.

Mkuu wa jeshi la polisi mkoani Kigoma kamishina msaidizi wa polisi George Mayunga alipoulizwa kuhusu uharamia huo wa ziwani Tanganyika alisema kuwa, takribani matukio makubwa matano ya uharamia yametokea katika kipindi cha miezi sita na kwamba wapo maharamia wanaoshikiria kwa uchunguzi ili kulibaini kundi lao.

Mkuu wa polisi kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai mkoa wa Kigoma Mrakibu mwandamizi wa Polisi Bw. Joseph Konyo anatoa taarifa kwa niaba ya mkuu wa polisi mkoa wa Kigoma, kwamba mwezi june mwaka huu matukio makubwa mawili ya uporaji wa ingine ulifanyika na Jeshi lilifanikiwa kumkamata haramia mmoja kutoka jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ambaye hadi sasa yuko rumande akisubiri kujibu mashataka kadhaa ya kuingia nchini na kufanya uharamia.

“Tunayo mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunaukomesha uharamia na hivi karibuni tumeanza kufanya mazungumzo ya kiintelijensia baina yetu na serikali ya Burundi, kwa kushirikisha vikosi vya ulinzi na usalama na tayari yapo makubaliano kadhaa ambayo yamefikiwa hasa kuhusiana na ubadirishanaji wa taarifa za kiusalama” Anasema Joseph Konyo mkuu wa upelelezi mkoa wa Kigoma.

Hivi karibuni Rais
wa Tanzania Dr.
Jakaya Mrisho Kikwete alikuwa mkoani Kigoma kwa shughuli za kujinadi ili apatiwe fursa nyingine ya kuiongaza Jamhuri ya muungano wa Tanzania, na katika ahadi zake alieleza kuwepo kwa mikakati ya kupambana na maharamia ndani ya ziwa Tanganyika.

Rais Kikwete alieleza kuwa, tayari serikali za Tanzania na Marekani zimeingia katika ushirikiano kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa askari za kikosi cha doria katika ziwa Tanganyika, Victoria na Bahari ya hindi kwa lengo la kukomesha uharamia unaoendelea hadi sasa.

Alieleza kuwa tayari askari kadhaa wamesafirishwa kwenda marekani kwa ajili ya mafunzo na serikali inatengeneza Boti kadhaa kwa ajil ya shughuli za ulinzi na usalama katika maziwa hayo mawili ya kasikazini Magharibi mwa Tanzania.

Pamoja na shughuli nyingine za kilimo na ufugaji, wakazi wa mkoa wa kigoma hususani wilaya za Kigoma vijijini na Kigoma mjini wanalitegemea ziwa Tanganyika kwa shughuli za kiuchumi hususani uvuaji wa dagaa na samaki aina ya mgebuka, hivyo endapo ulinzi hautaimarishwa ni wazi kuwa uchumi wa wavuvi na wafanyabiashara wanaolitumia ziwa hilo kwa shughuli za usafiri na usafirishaji utaporomoka.


No comments:

Post a Comment