Saturday, September 18, 2010

MABOMU YA KIVITA YAKUTWA KATIKA MAKAZI YA WATU KIGOMA


Mabomu mawili ya kutupwa kwa mkono yameokotwa jana katika mtaa wa Mwenge kata ya Gungu mjini Kigoma yakiwa yamehifadhiwa juu ya mti wa Mrumba ulio katikati ya nyumba tatu katika eneo hilo .

Mashuhuda wa tukio hilo ,wamesema mabomu hayo yaligunduliwa na vijana wawili waliopewa kazi ya kukata mti huo, ambapo wakiwa wanaendelea na kazi hiyo waligundua kuwepo kwa mfuko uliopachikwa katika moja ya matawi.

Shuhuda huyo Bakili Mohamed  amesema baada ya kuona mfuko huo,waliushika na kuushusha chini lakini hawakuvitambua vitu vilivyokuwemo hadi watu walipokusanyika zaidi na kugundua kuwa ni mabomu,hali iliyofanya waite polisi.

“Leo ilikuwa mwisho wa uhai wetu,tumeyashikashika kwa mikono kidogo,na hatukujua kama ni mabomu hadi alipokuja mama mmoja na kusema hiyo ni hatari hayo ni mabomu nyie vijana iteni polisi haraka tutakufa wote”alisema Bakili.

Baada ya kupata taarifa hiyo,jeshi la polisi lilitoa taarifa kwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania JWTZ ambao walifika katika eneo hilo na kuyachukua mabomu hayo ambayo yalikuwa bado hayajalipuka.

Mti yalipokutwa mabomu hayo upo katikati ya nyumba ya Hamidu Mohamed,Isabela January na Kani Okange,ambapo vijana hao walipewa kazi ya kukata mti huo na mmoja wa wamiliki wa nyumba hizo Hamidu Mohamed.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kigoma George Mayunga amesema jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na kwamba limewahoji vijana wawili Bakila Mohamed na Yahya Ramadhan ambao walipewa kazi ya kukata mti huo na kuwaachia.

“Tunawashukuru sana wananchi,wameona vitu wasivyovifamu na wametuarifu haraka na sisi tumechukua hatua zinazostahili bila kuchelewa kwa kushirikiana na wenzetu wa Jeshi la Wananchi”alisema kamanda Mayunga.

Hata hivyo amesema polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini chanzo cha mabomu hayo kuhifadhiwa katika mti huo.


Na. Propser Kwigize, Kigoma leo

No comments:

Post a Comment